Wahamiaji sita kutoka Afrika waliokuwa wakijaribu kuvuka kuingia Israel kupitia jangwa la Sinai nchini Misri wameuawa.
Maafisa usalama wa Misri wamesema wanne kati ya wahamiaji hao waliuawa na watu waliokuwa wakiwasafirisha kuwapeleka Israel kufuatia kufarakana nao.
Wengine wawili wameuawa na maafisa wanaolinda mpaka wa Misri, wakati wakijaribu kuingia Israel.
Wanaharakati wa haki za binaadam, wameishutumu Misri kwa mauaji ya wahamiaji wengi katika mpaka huo katika miaka michache iliyopita.
Wahamiaji wengi, wanaotafuta ukimbizi wa kisiasa au ajira nchini Israel, wanatokea Sudan na katika Pembe ya Afrika.
Afisa usalama wa Misri ameliambia shirika la habari la AFP kuwa waafrika hao sita waliouawa siku ya Ijumaa walikuwa wakitokea Eritrea.
Wahamiaji wamesema mzozo kati ya wahamiaji hao na wanaowasafirisha ulizuka, baada ya wasafirishaji hao kudai fedha zaidi za kuwapeleka Israel.
Baadhi ya wahamiaji walipora silaha kutoka kwa wasafirishaji na kuanza kurushiana risasi, ambapo wahamiaji wanne walikufa.
Kundi la wahamiaji lilisambaratika, ambao wawili baadaye walipigwa risasi mpakani.
Wahamiaji wasiopungua 17 walikamatwa na polisi wa Misri, maafisa wamesema.
No comments:
Post a Comment