Kanisa moja la mjini Florida nchini Marekani limetangaza mpango wake wa kuchoma moto quran siku ya septemba 11 katika kuadhimisha miaka minane baada ya mashambulizi ya mabomu nchini Marekani.
Katika matangazo yaliyowekwa kwenye mtandao wa Facebook, kanisa la The Dove World Outreach Center lililopo kwenye kitongoji cha Gainesville, Florida nchini Marekani limetangaza mpango wa kuichoma moto quran ili kuonyesha upinzani kwa uislamu na kuonyesha kuwa uislamu ni dini ya mashetani.
Kampeni ya kanisa hilo katika mtandao wa Facebook imeishapata watu 1,500 ambao wameunga mkono kampeni hiyo lakini pia kanisa hilo limetumiwa vitisho vingi toka kwa waislamu.
Mchungaji wa kanisa hilo, Terry Jones ambaye alitoa kitabu cha kuukashifu uislamu kinachoitwa "Islam is of The Devil" ametoa fulana ambazo zimeandikwa maandishi hayo ambayo yamesababisha mtafaruku.
"Uislamu na sheria za kiislamu ndio sababu za mashambulizi ya septemba 11", alisema mchungaji Jones akiongea na shirika la habari la AFP.
"Tutazichoma moto quran kwasababu tunafikiri huu ni wakati wa wakristo, makanisa na wanasiasa kusimama pamoja na kusema hapana kwa Uislamu, Uislamu na sheria za kiislamu hazikaribishwi hapa Marekani", alisema mchungaji Jones.
"Tumetumiwa vitisho vingi vya kuuliwa toka kwa makundi ya Jihad lakini hatuwezi kuwa waoga na kuzificha imani zetu", aliendelea kusema mchungaji Jones.
Hata hivyo, Umoja wa makanisa nchini Marekani The National Association of Evangelicals (NAE) umeitisha mwito wa kulitaka kanisa hilo kuufuta mpango wake wa kuzichoma moto quran.
"Inaonekana kama vile kuzichoma moto quran ni kulipa kisasi", alisema rais wa NAE, Leith Anderson.
"Lakini biblia inasema kuwa wakristo hawapaswi kulipa ubaya kwa ubaya bali kujaribu kuonyesha wema kati yao na kwa watu wote", alisema rais huyo wa makanisa Marekani.
Makundi ya waislamu nchini Marekani yamelaani mpango huo wa kanisa la Gainesville.
"Kwa bahati mbaya ndani ya Florida na Marekani kwa ujumla, uislamu unaenea kwa kasi", msemaji wa baraza la mahusiano ya wamarekani waislamu, Ramsey Kilic alisema.
"Hatutaki kuchukua hatua yoyote ili kuepusha shari, tunajua wanachotafuta ni umaarufu tu", alimalizia kusema Kilic.
No comments:
Post a Comment