Nahodha wa timu kubwa ya Brazili ya Flamengo ambayo ilitwaa ubingwa wa ligi kuu ya Brazili mwaka jana anashikiliwa na polisi kwa kumuua mpenzi wake wa zamani na kisha kumlisha mbwa maiti yake.
Bruno Fernandes das Dores de Souza, 25 au maarufu nchini Brazili kama Bruno ambaye alikuwa nahodha wa timu maarufu kuliko zote nchini Brazili ya Flamengo, anashikiliwa na polisi kwa mauaji ya mpenzi wake wa zamani Eliza Samudio, 25 ambaye alikuwa ni mrembo mwanamitindo.
Eliza alitoweka mwezi uliopita baada ya kumfikisha mahakamani Bruno kwa kuikataa mimba aliyompachika. Eliza alikuwa na mimba ya miezi minne na alikuwa akidai kuwa Bruno ndio baba.
Wakili wa Eliza aliiomba mahakama imkamate Bruno ambaye naye aliingia mitini baada ya mahakama kuidhinisha amri ya kumtia mbaroni.
Bruno alijisalimisha mwenyewe polisi baada ya kujificha kwa muda mrefu.
Ukatili wa Bruno ambaye hivi sasa amemuoa mwanamke mwingine, uliwekwa wazi na binamu wa mkewe ambaye aliiambia polisi kuwa alishiriki katika kumteka Eliza kabla ya kumuua.
Taarifa zilisema kuwa Eliza alitekwa mjini Rio de Janeiro na kupelekwa katika mji wa Belo Horizonte ambako aliuliwa kwa kunyongwa na kisha mwili wake kugawanywa sehemu tatu na kupewa mbwa wale. Vipande vilivyobaki vilizikwa chini ya zege.
Mke wa Bruno, Dayane Souza naye ametiwa mbaroni pamoja na marafiki kadhaa wa Bruno wakihusishwa na kutoweka kwa Eliza.
Klabu ya Flamengo imemfukuza Bruno ambaye aliichezea timu hiyo kuanzia mwaka 2006 na alikuwa nahodha mwaka jana wakati timu hiyo ilipotwaa ubingwa wa Brazil.
No comments:
Post a Comment