Dini ni mfumo wa maishani
Friday, September 17, 2010
Ufaransa na Burka:Ujerumani na riba za mabenki.
Vipi Kuba kujinusuru na msukosuko wa uchumi wake ?
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamechambua mada mbali mbali tangu za ndani hata za nje ya nchi: Ufaransa na Burka,Kuba na mkakati wake mpya wa mageuzi ya uchumi-ni miongoni mwa mada za nje.Lakini pia, hali inayojikuta sasa serikali ya Ujerumani ya kanzela Merkel na jinsi mabenki nchini yanavyotoza riba kubw kwa wateja wanaokopa.
Berliner zeitung na Kuba yageuza mkondo katika uchumi.Laandika:
Uchumi wa kisiwa cha Kuba, umekumbwa na msukosuko.Bidhaa zake inazouza n'gambo mwaka jana zilipungua kwa kima cha 36% wakati huo huo mavuno ya miwa inayotengezewa zao lake la sukari yalikuwa mabaya kabisa tangu 1905.
Sasa Rais Raul Castro, anajaribu kuzuwia kuporomoka kwa Kuba, lakini kwa muda mrefu ujao, uchumi wa Kuba unaweza tu kuokolewa endapo pakifanyika mageuzi ya sarafu na kuruhusu kumiminika fedha za kigeni nchini.
Mageuzi kama hayo lakini, hayaendi sambamba na mfumo wa kidikteta .Na hiyo ndio inayoifanya Kuba kutojua njia gani kufuata:Kuba, inajikuta chini ya udiktetea wa Castro ambao unawekea mipaka mageuzi yanayofanyika sasa."
Likituchukua Ufaransa na sera za Rais Sarkozy za kupiga marufuku Burka-aina ya bui-bui linalofunika mwili mzima isipokuwa macho tu, gazeti la Saarbrücker Zeitung-laandika:
"Kwa kupiga marufuku Burka, Sarkozy na serikali yake hawakulenga hasa kuweka nidhamu nchini,bali hasa kuvutia kura za wafuasi wa mrengo wa kulia .Kuwatimua nchini kwa Waroma,si kingine bali, ni saifisha-safisha ya kikabila na kunafanya kupigwa marufuku kwa Burka kuonekane kwa jicho jengine kabisa.
Rais huyo wa Ufaransa, anafuata mkondo mkali wa kuitenga na kuisafisha nchi yake na raia wa kigeni ambao, hapo kabla, aliwatumia kama kisingizo kwa kushindwa kufanya kazi sera zake."
Sarkozy, laongeza Saarbrücker Zeitung,amevuka mpaka ambao ila zilizotolewa na miji mikuu ya nchi jirani zimestahiki.
Frankfurter Allgemeine Zeitung likiendeleza mada hii na hasa juu ya kutimuliwa kwa waroma nchini Ufaransa, laandika:
"Changamoto hii ya kuoneshana nguvu, kamwe Ufaransa haiwezi kushinda.Kwani, hivi sasa sio tena ni mvutano kati ya serikali ya Ufaransa na maalfu ya waroma kutoka Rumania na Bulgaria,bali kwanza ni kesi ya kisiasa na sio ya kisheria na Tume ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Jamhuri ya Ufaransa...."
Ama kuhusu hali jumla inayojikuta sasa serikali ya Ujerumani ya kanzela Angela Merkel, gazeti la Augsburger Allgemeine laandika:
"Tangu pale vyama vya CDU/CSU na cha kiliberal (FDP) kutawala pamoja, vimejitwika pia jukumu la upinzani.Katika maswali mbali mbali kuanzia kodi,Hartz IV ,bima ya afya na jukumu la kulitumikia jeshi,kumekuwa na mawazo tofauti .
Kwa wakati fulani, ikibainika kana kwamba ,kiongozi wa Upinzani kutoka chama cha SPD, hakalii kiti cha usoni upande wa wabunge wake,bali katika Afisi ya waziri-mkuu mjini Munich.Waziri mkuu wa ( Bavaria )Horst Seehoefer , anahujumu kile ambacho binafsi, wakati wa majadiliano ya kuunda serikali aliichangia kuridhia."
Mwishoe, gazeti la Rhein-Neckar-zeitung linatumalizia kwa kuchambua riba kubwa mno inayotozwa na mabenki Ujerumani kwa wale wanaokopa kupindukia hazina iliomo katika akiba zao .Laandika:
"Kwa mabenki yanayotoa mikopo hiyo, ni biashara nono kabisa.Kwani, kila mjerumani wa 6 ana kasoro katika akiba yake.Wakati huo huo lakini, mabenki hujipatia fedha yanazokopesha, kwa riba ndogo.Kwamba, hali hii imezifedhehi sasa Banki,ni kuona nyingi zimefuta ghafula katika mtandao wao matangazo yao ya mikopo.........."
Mwandishi: Ramadhan Ali/ DPA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment