Dini ni mfumo wa maishani

Dini ni mfumo wa maishani

Monday, January 24, 2011

Wingu zito Anglikana




Mussa Mwangoka, Sumbawanga
na Minael Msuya, Dar

MGOGORO umezidi kutikisa Kanisa Anglikana nchini (KAT) baada ya waliotengwa na kisha nao kuanzisha Kanisa Anglikana la Kiinjili Tanzania (KAKT), kutia ngumu wakisema wataendelea kuhibiri Injili.

Wakati wafuasi wa KATK wakitunisha misuli, waumini wa KAT katika Kanisa la Watiifu Wote katika Jimbo la Ziwa Rukwa mjini Sumbawanga, wamemzuia Askofu wao kuendesha ibada wakisema , "Hawamtambui,'" na kumlazimu kukaa juu ya gogo kwenye kivuli mbele ya kanisa huku akiwa amevalia Kiaskofu.

Matukio hayo yaliyotokea jana kwenye maeneo mbalimbali na kwa nyakati tofauti, ni muendelezo wa mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu na kusababisha kutotambuliwa na kufukuzwa kwa baadhi ya maaskofu.

Katika kile kinachoashiria kuendelea kwa mgogoro huo, waumini wa KAT jimbo hilo la Ziwa Rukwa Sumbawanga, walimzuia Askofu Canon Kasagara na wafuasi wake,
wakisisitiza hafai kuwa kiongozi wao wa kiroho.

Waumini hao katika kutimiza mpango mkakati wao wa kumzuia Askofu Kasagara, walilazimika kukaa kutwa nzima kanisani wakifanya ibada ya misa ya Jumapili.

Kutokana na waumini hao kumzuia, Askofu huyo alilazimika kuketi juu ya gogo chini ya kivuli cha mti mbele ya kanisa hilo akiwa amevalia mavazi hayo ya Kiaskofu na mkononi akiwa ameshikilia fimbo ya kichungaji.

Awali, inadaiwa Askofu huyo alikutana na OCD wa Sumbawanga, Mohamedi Mbonde, na kumsihi asiende kanisani hapo kwani hali ni tete baada ya waumini wa kanisa hilo kudai hawamtambui na hawatamruhusu kuingia kanisani humo, lakini alikaidi.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Sumbawanga, Salum Shilingi alithibitisha hayo huku akidai kuwa mkuu wa wilaya hiyo, John Mzurikwao, ambaye alikuwa amepewa mwaliko na Askofu Kasagara wa kuhudhuria ibada kanisani hapo alishindwa kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni 'busara'.

Ibada ya Misa iliendela kwa utulivu huku kanisa hilo lilikuwa limefurika waumini ambao Mchungaji mstaafu John Mazingaliwa, aliwataka waumini wenzake wawe na moyo wa ushupavu kufia dini yao kwa kutetea haki yao.

Inadaiwa kanisa hilo huwa na ibada moja tu ya Misa Takatifu, ambayo huaanza saa tatu.

Kabla ya tukio, Askofu Kasagara ambaye kwa miezi saba aliweka makao yake mjini Mpanda baada ya waumini wa kanisa hilo kumkataa aliongozana na wana kwaya kutoka Mpanda mjini na wachungaji wapatao 17 kutoka makanisa ya Namanyere, Mpanda Mjini, Mishamo na Nduruma na aliwasili kwenye viwanja vya kanisa hilo saa sita mchana.

Lakini, baada ya kutua alijikuta akigonga ukuta baada ya waumini wengi na uongozi wa kanisa hilo kugoma kumruhusu kuingia kanisani humo kufanya ibada kwa madai hayo ya kutomtambua kwa madai uchaguzi wake haukuwa sahihi.


Akizungumzia sakata hilo Katibu Msaidizi wa Baraza la Wazee Wandi Joseph, alisema uongozi wa kanisa hilo ulimtaarifu na kumwomba Askofu wa Dayosisi ya Mbeya, John Mwela, ambaye aliwasiliana na Askofu Kasagara na kumsihi asifanye ziara ya kutembela kanisa hilo, lakini inadaiwa pia alikaidi.

Wakati ibada ikiendelea kanisani humo, baadhi ya waumini wanaomuunga mkono Askofu Kasagara ambao ni wachahe, hawakuingia kanisani waliishia kukaa nje makundi kwa makundi na maafisa usalama na askari polisi, walikuwa wakifuatilia sakata hilo kwa karibu.

Muda mfupi baadae askari wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa na silaha waliwasili kanisani hapo hali ilyowafanya baadhi ya waumini hasa akina mama na watoto waliokuwa ndani ya kukatiza ibada na kutoka nje kwa hofu ya maisha yao huku wale waliokula kiapo cha kufia dini wakiendelea na ibada bila ya hofu.

Akizungumzia sakata la kutomkubali Askofu Kasagara, Mwenyekiti wa baraza la Wazee wa kanisa hilo mjini Sumbawanga John Mwambasa, alisema Askofu Mkuu Dk Valentine Mokiwa pamoja na kukubali kutomsimika Askofu huyo, lakini alilazimika kumsimika kutokana na shinikizo alilopewa na Askofu Mkuu Mstafu Gerald Mpango.

Akizungumzia sakata hilo Askofu Kasagara, akiwa amezungukwa na umati mkubwa nje ya jengo la kanisa hilo aliwaeleza waandishi wa habari kama baadhi ya waumini hao wanamkataa wana sababu zao, lakini aliwataka wajitenge na waabudu mahali pengine na yuko tayari kuwapatia msaada wowote ule watakaouhitaji.

Hadi gazeti hili linaenda mtamboni bado, Askofu huyo alikuwa nje na ujumbe wake huku waumini wa kanisa hilo wakiendelea kuimba, kusali na kumuabudu Mungu.

Wakati huo huo Askofu wa KAKT Ainea Kusenha, alisema kanisa hilo litaendelelea kuhubiri Injili licha ya Askofu Dk Mokiwa kutoa hadhari kwa waumini wake kutojiunga na kanisa hilo.

Kusenha aliitoa kauli hiyo jana alipokuwa katika ibada ya Jumapili iliyofanyika katika kanisa la Anglikana Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Ibada hiyo iliandaliwa maalumu kwa ajili ya kuwatoa hofu waumini wadhehebu hilo unaohusu mpasuko wa kanisa la Anglikana duniani.

“Katika kipindi cha muda mrefu sisi viongozi wa Kanisa la Anglikana tumekuwa na malumbano ya hapa na pale na kufikia hata hatua ya kujigawa," alisema na kuongeza:,

..Binafsi sikuwahi kufikiri kama ningeweza kufanya mgawanyiko huu lakini nilipogundua kuwa viongozi wetu wakubwa wanakanyaga katiba ya dini, niliamua kuomba usajili wa kanisa hili.”

“Ibada yangu ya leo nimeamua kuipa kichwa cha somo hili ‘Hayuko Wasalama’ ikiwa na maana kuwa, jamii na Taifa la Tanzania kwa ujumla haliko salama. Taifa linapita katika kipindi kigumu cha mabadiliko kutokana na dhambi ya watu wachache au mtu mmoja.”

Alifafanua kwamba, kanisa Anglikana limekuwa likihubiri na kuwapotosha waumini wake kutokana na na kukanyaga katiba ya dini chini badala ya kuitekeleza kama walivyoapa na kwamba wanaunga mkono matendo ambayo ni dhambi kwa Mungu.

Kwa msisitizo, Askofu Kusenha alisema baada ya kuomba usajili wa kanisa la anglikana Injili Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Valentino Mokiwa aliandika barua kwa makanisa mbalimabli ili kuzuia usajili huo na kuwa wanaojiita Anglikana injili ni wahuni.

“Haya yote yanachangia viongozi wa dini kushindwa kuionya serikali kwakuwa hakuna aliye msafi. kinachotakiwa hapa ni kila mtu kujisafisha ili sisi na nchi yetu kwa ujumla turudi katika mstari wa Mungu,” alisisitiza.

Huo ni mgogoro mwingine unaolikumba kanisa hilo baada ya muda mrefu kutikiswa na kashfa ya ushoga inayokabili maaskofu wake ikiwemo nchini Uingereza, ambako ndiko makao makuu duniani.

No comments:

Post a Comment