Dini ni mfumo wa maishani
Monday, November 22, 2010
Viongozi wa dini wamtuliza Dk Slaa
Salim Said
JOPO la viongozi wa dini limefanya ziara ya ghafla kwa aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Wiilibrod Slaa na kumtaka akubali matokeo au atumie njia za kisheria kudai haki yake, Mwananchi imebaini.
Dk Slaa hakutokea kwenye hafla ya kutangaza mshindi wa kiti cha urais wala sherehe za kuapishwa kwa Jakaya Kikwete kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano na aliahidi kuwa angetoa tamko zito jana.
Wakati Tume ya Uchaguzi (Nec) ikiendelea kutangaza matokeo, Dk Slaa aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa hangekubaliana na matokeo kutokana na kubaini kuwa Nec ilikuwa inatangaza matokeo tofauti na yaliyo kwenye nyaraka walizosaini na hivyo kuitaka isitishe zoezi hilo ili kura zianza kuhesabiwa upya.
Dk Slaa pia aliituhumu Idara ya Usalama wa Taifa kuwa ilihusika kuchakachua kura kwa lengo la kumbeba mgombea mmoja wa urais, tuhuma ambazo ziliifanya taasisi hiyo, inayofanya kazi kwa siri, ijitokeze hadharani kujibu na kumuelezea katibu huyo mkuu wa Chadema kuwa "ni mzushi".
Tamko hilo la Dk Slaa lilionekana kuwashutua viongozi wa dini na kuhisi dalili za kutokea mvutano ambao ungeweza kusababisha kuvunjika kwa amani. Mwananchi imebaini kuwa ziara ya kimya kimya ya viongozi hao wa dini ilifanywa wiki iliyopita kabla ya Nec kumtangaza Kikwete kuwa ni mshindi.
Kwa mujibu wa habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kwamba viongozi hao walimtaka Dk Slaa asisababisha mvutano ili kudumisha amani ya nchi. Habari za ziara hiyo ya dharura ya jopo hilo la viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zilithibitishwa na meneja wa kampeni wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu. Profesa Baregu aliiambia Mwananchi kuwa ujumbe mkubwa uliofikishwa na jopo hilo ulikuwa ni kuwaomba viongozi wa Chadema kutumia njia sahihi za kudai haki yao ambazo hazitazusha vurugu, fujo wala uvunjifu wowote wa amani.
“Ujumbe wao kwetu ulikuwa ni kutuomba kwamba kusiwe na vurugu, fujo wala uvunjifu wowote wa amani wakati wa kutangazwa matokeo na hata baada ya kutangazwa,” alisema Profesa Baregu. “Badala yake wakatuomba kama hatujaridhika na matokeo basi tutumie taratibu za kisheria zilizowekwa kudai haki. Lakini sisi tuliwaeleza kuwa hatuna nia ya kufanya vurugu wala kuandamana, lakini uchaguzi umevurugwa na hatuwezi kukubali.”
Alisema jopo la viongozi hao wanne wa dini wakiongozwa na askofu mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa lilifanya ziara hiyo baada ya Chadema kuitaka Nec kusitisha utangazaji wa matokeo kwa kuwa Usalama wa Taifa wamechakachua matokeo.
“Sijui walikuwa na wasiwasi gani au nani aliwashauri kuja tena kuonana na viongozi wa Chadema, lakini nadhani ni baada ya kuona tumesema hatungekubali matokeo kwa kuwa uchaguzi umechafuliwa,” alisema Profesa Baregu. Alisema pamoja na wasiwasi huo wa viongozi wa dini, Chadema haikuwa na mpango wowote wa kuunganisha nguvu ya umma na kuingia barabarani, kama ilivyofanyika Kenya, kudai haki. “Lakini hatujaridhika na matokeo kwa sababu uchaguzi ulikuwa mchafu.
Rais amechaguliwa na robo tu ya wapigakura. Nec imeongeza majina kwa sababu kabla ya uchaguzi ilisema wapigakura wote ni 19.9 milioni, lakini akitangaza mshindi Jaji Lewis Makame anasema ni 20.1, hatujui wametoka wapi,” alisema Profesa Baregu. Kwa mujibu wa Baregu wengine waliokuwamo katika msafara huo wa viongozi wa dini walikuwa ni kutoka Kanisa Katoliki na Baraza Kuu la Waislaam Tanzania (Bakwata).
Dk Slaa, ambaye alishika nafasi ya pili kwenye kinyang'anyiro cha urais kwa kupata asilimia 26 ya kura, pia alitembelewa na jopo la viongozi wa dini kabla ya kumalizika kwa kampeni wakimtaka awe tayari kupokea matokeo yoyote yale. Jopo hilo lilidai wakati huo kuwa lingetembelea wagombea wengine wa urais, lakini halikufanya tena ziara kwa wagombea wengine hadi uchaguzi ulipofanyika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment