Yesu alikuwa Myahudi mwanamume aliyeishi miaka 2000 hivi iliyopita (labda 6 KK - 30 B.K.).
Kutokana na umuhimu wake katika historia ya binadamu, kwa kawaida miaka yote inahesabiwa kwanzia ujio wake (ulivyokadiriwa kimakosa katika karne ya 6).
Mazingira yake
Nchi ambayo Yesu alizaliwa akafundisha ni nchi ileile ambayo Mungu aliwaahidia Waisraeli tangu zamani za Abrahamu, ni nchi ileile waliyoiteka chini ya Yoshua, ni nchi ileile waliyoirudia kutoka utumwani Babeli.
Lakini wakati wote wa Agano Jipya, yaani tangu Yesu alipozaliwa hadi mwisho wa maisha ya mitume wake, nchi hiyo haikuwa huru, bali chini ya himaya ya Warumi, ingawa pengine hao waliwakabidhi vibaraka, yaani watawala wenyeji waliowekwa na wakoloni.
Vibaraka hao ni Herode Mkuu (37 KK-4 KK) na wazawa wake, ambao tena hawakuwa Waisraeli halisi bali Waedomu ingawa kabila lao lililazimishwa kuingia dini ya Kiyahudi karne iliyotangulia. Ukoo huo unajulikana kwa ukatili, uchu wa madaraka na uzinifu wake.
Vilevile maliwali wa Kirumi waliowekwa pengine kutawala nchi au sehemu fulani walionyesha mara nyingi ukatili na dharau kwa Waisraeli na dini yao, hata kusababisha chuki na mapigano kati ya jeshi na wananchi. Mfano mmojawapo ni Ponsyo Pilato aliyesimamia Uyahudi kuanzia mwaka 26 hadi 36 B.K.
Mbali na hayo, utawala wa Roma, ulioenea Ulaya Magharibi na Kusini, Afrika Kaskazini na nchi za Mashariki ya Kati kupakana na Iraq ya leo, kwa jumla ulihakikisha hali ya amani kwa muda wote wa Agano Jipya na karne za kwanza za Kanisa. Hali hiyo, pamoja na umoja wa dola hilo lote, na urahisi wa mawasiliano kwa njia ya barabara zilizotengenezwa na Warumi, na uenezi wa lugha ya kimataifa (Kiyunani yaani Kigiriki cha zamani), ilichangia kasi ya uenezaji wa habari njema (Injili). Lugha hiyo ndiyo iliyotumiwa na waandishi wote wa Agano Jipya ili vitabu vyao viwafaidishe watu wengi zaidi, ingawa baadhi yao hawakuijua vizuri.
Lugha asili ya Yesu na ya Mitume ilikuwa Kiaramu ambacho ni jamii ya Kiyahudi na ambacho polepole kilishika nafasi yake kati ya Wayahudi kuanzia karne ya sita K.K. Hao wote walitokea mkoa wa Galilaya, uliokuwa na mchanganyiko wa watu (Waisraeli na mataifa), kiasi kwamba huko Wayahudi wenyewe walifuata kwa urahisi desturi za Kiyunani hata wakadharauliwa na wenzao wa Kusini (Yerusalemu na mkoa wa Yudea).
Kati ya mikoa hiyo miwili ulienea mkoa wa Samaria ambao wakazi wake walijenga uadui mkubwa na Wayahudi baada ya uhamisho wa Babeli, walipokataliwa kuchangia ujenzi wa hekalu la pili la Yerusalemu.
[hariri] Maisha yake
Dionisi Mdogo, mmonaki aliyeanzisha (mwaka 533 hivi) mtindo wa kuhesabu miaka kuanzia kuzaliwa Yesu kurudi nyuma (K.K.) au kwenda mbele (B.K.), alikosea hesabu zake. Leo tunakisia Yesu alizaliwa mwaka 6 hivi K.K. kwa sababu alizaliwa Bethlehemu chini ya Herode Mkuu aliyefariki mwaka 4 K.K.
Huyo alipojaribu kumuua mtoto Yesu, familia takatifu ilikimbilia Misri mpaka baada ya kufa kwake. Hapo ikarudi Galilaya hata Yesu akajulikana kwa jina la kijiji cha Nazareti kilichodharauliwa na Wagalilaya pia. Ndipo alipokulia na kuishi akifanya kazi ya ufundi.
Mwaka 26 hivi B.K. ndugu yake Yohane Mbatizaji aliacha maisha ya jangwani na kuanza kuhubiri toba kandokando ya mto Yordani. Kwa kuwa Waisraeli walikosa manabii kwa muda mrefu, na walitamani sana ukombozi, walimuendea kwa wingi hata wakamtia hofu Herode Antipa.
Ingawa huyo akamfunga mapema akamuua, kazi ya Yohane ilikuwa imetimia kwa sababu aliweza kuwaandaa Waisraeli wengi (hasa watu wadogo na wakosefu) wampokee Yesu aliyebatizwa naye. Katika nafasi hiyo Yohane alimtambulisha kama Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu.
Ndipo Yesu naye alipoanza kuhubiri, lakini pia kutenda miujiza ya kila aina, akapata haraka wafuasi wengi. Kati yao akachagua Mitume wake 12 kama msingi mpya wa taifa la Mungu. Alifanya kazi hizo kuanzia Galilaya, akitangaza ujio wa ufalme wa Mungu, kwa maana ya kwamba ufalme uliotazamiwa na Wayahudi umewajia kwa njia yake.
Ingawa hakupitia shule yoyote ya Biblia, Yesu alionekana anafundisha vizuri kuliko walimu wa sheria wa kawaida, kama mtu mwenye mamlaka juu ya Torati. Mafundisho yake yalilingana na yale ya Mafarisayo kuliko na yale ya Masadukayo, lakini alishindana pia na hao wa kwanza.
Kijicho na upinzani vikazidi hasa Yerusalemu, walipoanza kufanya njama za kumuua. Ingawa Yesu alijua hayo, alijikaza kwenda katika mji mtakatifu autangazie habari njema na kufia huko. Baada ya kupokewa kwa shangwe kabla ya sherehe ya Pasaka ya mwaka 30 (au 33) akakamatwa na baraza la Israeli kwa tuhuma ya kufuru ya kujilinganisha na Mungu, halafu akakabidhiwa kwa liwali wa Kirumi aliyekuwa na mamlaka ya kutoa adhabu ya kifo. Baada ya kikao ambapo Wayahudi walitafuta kisingizio cha kisiasa, Ponsyo Pilato akalazimika kuagiza Yesu asulubiwe, na kisha kufa kwake kaburi lilindwe na askari.
Hata hivyo siku ya tatu kaburi likaonekana tupu, na Yesu akaanza kuwatokea wanafunzi wake wa kike na wa kiume kwa muda wa siku arubaini, halafu akapaa mbinguni mbele ya macho yao.
Habari hizo zikatangazwa kwa sauti tu kwa miaka kadhaa, halafu zikaanza kuandikwa. Kanisa linaheshimu kwa namna ya pekee, kama ushuhuda mkuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu na kama moyo wa Maandiko matakatifu yote, Injili nne zilizoandikwa na Marko, Mathayo, Mwinjili Luka na Yohane kati ya mwaka 65 na 100 hivi.
[hariri] Imani juu yake
Waumini wake wanaunda Kanisa la Kikristo ambalo linapatikana leo katika madhehebu mengi. Karibu wote wanamwamini kuwa Mungu aliyechukua umbile la mwanadamu au, kwa lugha nyingine, kuwa Mwana wa Mungu. Wakristo wengine wanaamini kuwa yeye ni mtume wa pekee wa Mungu ila sio Mungu.
Katika dini ya Uislamu, Yesu anajulikana kama Nabii Isa. Waislamu wanaamini kuwa yeye alikuwa ni nabii wa Mungu ila hakuwa mwana wa Mungu wala Mungu.
[hariri] Maadhimisho yake
Maisha yake yamekuwa msingi wa sikukuu mbalimbali zinazosheherekewa katika nchi nyingi duniani, kama vile Noeli auKrismasi (kuzaliwa kwake), Epifania (kuonekana kwake na kubatizwa kwake), Majilio (kuandaliwa ujio wake), Kwaresima (mafungo na mateso yake), Ijumaa Kuu (kifo chake); muhimu kuliko zote ni Pasaka (kufufuka kwake).
[hariri] Misingi ya ujuzi wetu juu yake
Yesu hakuacha maandiko yoyote. Habari zake zinapatikana hasa katika Biblia, kwa namna ya pekee katika Injili.
Nje ya Ukristo kuna habari fupi kuhusu Yesu katika maandiko ya waandishi Waroma, Wagiriki na Wayahudi. Habari hizi zinaangaliwa sana kwa sababu zimetungwa na watu wasiomwamini Yesu. Kwa ujumla zinathibitisha ya kwamba Yesu alikuwepo, alikuwa na wafuasi huko Roma na ya kwamba awali Waroma hawakuelewa tofauti kati ya wafuasi wake na Wayahudi. Muhimu ni hasa:
1. Mtaalamu Myahudi Flavius Josephus aliandika mnamo 90 B.K. kitabu cha „Antiquitates Judaicae“ (Habari za historia ya Kiyahudi) akitaja kifo cha „Yakobo ndugu wa Yesu“ (sura ya 20, 200).
2. Mwandishi Mroma Tacitus aliandika mnamo mwaka 117 ya kwamba Kaisari Nero alishtaki kikundi cha “Chrestiani” ya kuwa wamechoma moto mji wa Roma. Aliongeza: “Mtu ambaye ni asili ya jina hili ni Chrestus aliyeuawa wakati wa Tiberio kwa amri ya Pontio Pilato” (Annales XV,44).
3. Mwandishi Mroma Svetonius alimtaja “Chrestos” katika kitabu chake juu ya maisha ya Kaisari Claudius (25,4) ya kwamba huyu amesababisha fujo kati ya Wayahudi wa Roma hivyo Kaisari aliwafukuza mjini.
4. Mwanasiasa Mroma Gaius Plinius Caecilius Secundus aliacha barua kadhaa zinazotaja Wakristo mnamo mwaka 100 B.K. Alimwuliza Kaisari Traianus jinsi ya kushughulikia Wakristo waliokataa kutoa sadaka mbele ya sanamu za Kaisari.
Krismasi (pia Noeli)
Krismasi (pia Noeli) ni sikukuu ambako Wakristo husheherekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Kwa kawaida husheherekewa tarehe 25 Desemba katika Ukristo wa magharibi na tarehe 6 Januari katika ule wa mashariki.
Historia ya Krismasi
Uchoraji wa Kiorthodoksi unaoonyesha kuzaliwa kwake Kristo. Yesu anaonekana amevikwa sanda na kulazwa kaburini, kwa maana alizaliwa ili atukomboe kwa kifo chake
Tarehe halisi ya kuzaliwa kwake Yesu haijulikani kwa sababu utamaduni wa Wayahudi wa wakati ule haukuwa na sherehe au kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa.
Lakini baadaye Ukristo ulienea katika Dola la Roma na kati ya mataifa yaliyokuwa na kawaida ya kuzingatia siku ya kuzaliwa. Hivyo ilijitokeza hamu ya kusheherekea pia sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo. Ndiyo asili ya Sikukuu ya Krismasi.
Tangu mwanzo wa karne ya 3 BK kuna kumbukumbu ya waandishi mbalimbali waliojadili tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.
Habari za kwanza kabisa za makadirio ya tarehe ya kuzaliwa kwake Yesu zinapatikana kutoka Misri mnamo mwaka 200. Mwandishi Mkristo Klemens wa Alexandria (kitabu cha Stromateis I, xxi) alilalamikia udadisi wa wataalamu kadhaa wa Misri waliodai kwamba wamekadiria tarehe hiyo katika mwezi Mei, wengine katika Aprili. Alisema pia kuwa kikundi cha Kikristo cha wafuasi wa Basilides huko Misri walisheherekea Epifania pamoja na kuzaliwa kwake Yesu tarehe 6 Januari.
Labda kadirio la tarehe ya Desemba 25 pia lina asili katika Misri. Kuanzia mwaka 200 (kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Sixtus Julius Africanus) tunasikia kwamba wataalamu wa Misri walifikiri tarehe 25 Machi ilikuwa tarehe ya kufa kwake Kristo na pia siku ya kuzaliwa kwake. Kwa kuongeza miezi tisa ya mimba inajitokeza 25 Desemba kama tarehe ya kuzaliwa.
Mwaka wa liturujia
Magharibi
Majilio
Krismasi
Kipindi cha Noeli
Mama wa Mungu
Epifania
Ubatizo wa Bwana
Kwaresima
Siku tatu kuu za Pasaka
Pasaka
Kupaa Bwana
Pentekoste
Kugeuka sura
Kipindi cha kawaida
Mashariki
Sikukuu ya msalaba
Mfungo wa Krismasi
Krismasi
Epifania
Kwaresima kuu
Pasaka
Pentekoste
Mfungo wa Mitume
Sherehe kuu
Kugeuka sura
Kulala kwa Mama wa Mungu
Ulinzi wa Mama wa Mungu
Inaonekana tarehe 25 Desemba ilijitokeza wakati huo. Kuna taarifa ya mwaka 204 kutoka Ipolito wa Roma kwamba tarehe 25 Desemba ilikuwa sikukuu ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo.
Wataalamu mbalimbali walidai kwamba Kanisa lilipachika sikukuu ya Kristo kwenye tarehe hiyo kwa nia ya kuchukua nafasi ya sikukuu ya jua kama mungu "Sol invictus". Lakini pengine mambo yalikwenda kinyume, yaani kwamba Makaisari walianzisha sikukuu hiyo halafu wakaipanga tarehe ya Krismasi ili kushindana na Ukristo uliokuwa bado chini ya dhuluma.
Aliyeingiza sikukuu ya Kuzaliwa Jua (Mitra) huko Roma ni Eliogabalus (kaisari kuanzia 218 hadi 222). Baadaye Aurelianus akaithibitisha rasmi mwaka 273, hatimate ikahamishiwa tarehe 25 Desemba. Wakati wa Licinius (308-324) sikukuu hiyo ilikuwa ikiadhimishwa bado tarehe 19 Desemba. (Taz. maandishi yaliyotajwa na Allan S. Hoey katika ukurasa 480 (rejeo 128) wa Official Policy towards Oriental Cults in the Roman Army, Transactions and Proceedings of the American Philological Association (70) 1939, pp 456-481).
Kutoka Roma, uliokuwa mji mkuu wa Dola la Roma, sherehe ya 25 Desemba ilienea kote katika Ukristo.
Wakristo wengi husheherekea tarehe 25 Desemba (Wakatoliki, Waprotestanti, sehemu ya Waorthodoksi). Kati ya Waorthodoksi kuna tarehe nyingine, hasa 6 Januari kutokana na tofauti katika kalenda.
Habari za Krismasi katika Biblia
Habari za Krismasi kama sherehe hazipatikani katika Biblia kwa sababu zilizotajwa hapa juu.
Lakini hasa vitabu viwili vya Agano Jipya vina habari za kuzaliwa kwake Yesu, yaani Injili za Mathayo na Luka.
Katika Injili ya Mathayo
Mathayo anasimulia habari hizo katika mlango wa kwanza kuanzia aya 18 na katika mlango wa pili.
Bikira Maria alipata mimba wakati alipokuwa mchumba wa Yosefu. Yosefu alitaka kumwacha lakini aliambiwa na malaika aanze kuishi naye na kumkubali mtoto kama wake kwa kumpa jina "Yesu".
Mamajusi kutoka mashariki waliwatembelea na kuwaletea zawadi kwa sababu waliona nyota ya pekee iliyokuwa kwao alama ya kuzaliwa kwa mfalme mpya katika Uyahudi ikawaongoza hadi Yerusalemu. Lakini walipompitia mfalme Herode Mkuu, huyo alikasirika akimwogopa mfalme mpya. Hata hivyo aliwaelekeza Bethehemu kadiri ya utabiri wa nabii Mika.
Yosefu alipata tena ujumbe kutoka kwa malaika akaondoka na mtoto na Maria kukimbilia Misri kabla ya askari wa Herode hawajaweza kumuua Yesu.
Baada ya kifo cha Herode walirudi kutoka Misri lakini hawakuenda tena Bethlehemu bali kuhamia Nazareti katika mkoa wa Galilaya.
Katika Injili ya Luka
Katika taarifa ya Luka (mlango wa 1 na 2) Maria alipokea huko Nazareti ujumbe wa malaika mkuu Gabrieli kwamba atapata mimba na mtoto wa pekee.
Yosefu na Maria walikwenda Bethlehemu kwa sababu ya sensa iliyowataka kwenda katika mji alikotokea Yosefu. Hapo Yesu alizaliwa katika hori la kulishia wanyama; wachungaji mabondeni walitangaziwa na malaika habari hiyo wakaja kumwona mtoto.
Baada ya kuzaliwa wazazi walimpeleka Yesu Yerusalemu katika hekalu kufuatana na sheria ya Agano la Kale (Kitabu cha Kutoka 13,2; 13,15) halafu wakarudi kwao Nazareti.
Habari za Krismasi katika Korani
Korani pia ina habari za kuzaliwa kwake Yesu (nabii Isa).
Sura ya tatu (Al Imran, 42-47) ina habari za tangazo la malaika kwa Bikira Mariamu zinazofanana na Luka 1.
Sura ya 19 (Mariamu, 16-34) inarudia tangazo la malaika kwa Mariamu na inasimulia kuzaliwa kwake Yesu chini ya mti wa mtende, halafu majadiliano kati ya Mariamu na ndugu zake. Mtoto mchanga Yesu akaanza kusema wakati wa kuzaliwa akimtetea mama yake dhidi ya ndugu zake.
Krismasi katika maisha ya binadamu
Watu wote ni wakosefu na kujenga mazingira maovu hata wanayakinai na kutamani wamuone mtu tofauti, yaani mwema na mtakatifu. Pengine wanadhani fulani ni mwema kabisa, kumbe siyo.
Haja hiyo inaturudia sisi: kwa nini nisiwe mimi mtu wa namna hiyo? Kwa nini nisianze na moja kama kwa kuzaliwa upya kabla sijawadai wengine? Zaidi tena, haja kuu ya binadamu ni kumuona Mungu mwenyewe: lakini wapi, lini, namna gani
Krismasi katika liturujia
Kama kawaida, imani na liturujia ya Kikristo zinaitikia haja za binadamu. Kipindi cha Noeli kinatimiza haja tulizozitaja, kwa kuwa anazaliwa mtu mpya kabisa ambaye anatuvutia kwa wema wake na ambaye tukimuona tumemuona Mungu, tena tukimpokea tunazaliwa upya kama wana wa Mungu.
“Leo amezaliwa kwa ajili yenu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana”. Tunapoadhimisha Noeli tangazo hilo la malaika kwa wachungaji linatufikia sisi. Si kujidanganya, kana kwamba Yesu angezaliwa leo, wala hatukumbuki tu tukio la zamani, bali fumbo la kuzaliwa Bwana linatufikia leo katika liturujia na kutuletea neema zake. Hivyo tunaweza tukazaliwa upya kwa kushiriki kuzaliwa kwa kichwa chetu.
Liturujia inashangilia hivi, “Lo! Mabadilishano ya ajabu! Mwana wa Mungu anakuwa mtu kusudi mtu awe mwana wa Mungu!”. Tena si binadamu tu, bali viumbe vyote vinapata heshima mpya kwa Neno wa milele kujifanya kiumbe
No comments:
Post a Comment