Dini ni mfumo wa maishani

Dini ni mfumo wa maishani

Sunday, December 19, 2010

KANISA Katoliki katika Jimbo la Sumbawanga, mkoani Rukwa, limevunja ukimya na kunena kuhusu mambo yaliyosababisha waumini wake, kutengwa



Mussa Mwangoka,
Sumbawanga

KANISA Katoliki katika Jimbo la Sumbawanga, mkoani Rukwa, limevunja ukimya na kunena kuhusu mambo yaliyosababisha waumini wake, kutengwa na wengine kuwekewa pingamizi kwa kukufuru utatu mtakatifu wakati wa uchaguzi mkuu, uliomalizika Oktoba 31 mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja siku kadhaa baada ya baadhi ya vyombo vya habari, kuandika na kuchapisha habari kuhusu sakata hilo huku kanisa likiwa halizungumzi lolote.

Kitendo hicho, kiliwafanya baadhiya wananchi waliowahi kusoma habari hizo kutaka kujua ukweli kuhusu madai kuwa kanisa, limewatenga baadhi ya waumini wake kwa kukufuru utatu mtakatifu wakati wa uchaguzi mkuu.

Jana, Wakili wa Kiaskofu katika Jimbo la Sumbawanga, Padri Modest Katonto, alikiri kuhusu adhabu hiyo kwa baadhi ya waumini wa kanisa hilo na kwamba hakuna anayeweza kuitengua.

"Kanisa lingependa ifahamike kuwa hakuna mamlaka yoyote ya kidunia, inayoweza kuwaoondolea waumini hao adhabu hiyo, isipokuwa kwa jitihada za mtu mwenyewe binafsi kujipatanisha na kanisa kwa wale waliotengwa," alisema Padri Katonto.
Kanisa hilo pia limesema halina itikadi za kisiasa na kwamba adhabu zimetolewa kwa waumini hao, hazijali wadhifa wa mtu yeyote katika jamii.

Alisema kilichozingatiwa ni makosa ya kwenda kinyume cha imani na kushabikia mafundisho potofu.

Wakili huyo wa kiaskofu, alisema waumini waliokumbwa na adhabu hizo wako katika makundi mawili na kwamba la kwanza, ni la waliotengwa kwa kosa la kujilinganisha na utatu mtakatifu na kushabikia mafundisho potofu, huku wakijua wazi kuwa kitendo hicho ni cha uovu.

Kwa mujibu wa Padri Katonto, kundi hilo lina jumla ya waumini 27.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya kanisa namba 1364, kosa lililofanywa na watu hao, linawatenga na umoja wa kanisa hata bila kutangaziwa au kujulishwa na kiongozi wa kanisa.

Alisema chini ya adhabu waliyopewa, waumini hao wamepoteza haki ya kushiriki katika idaba zote za hadhara za kanisa katoliki, kutoshiriki katika maadhimisho ya sakramenti, kutopokea akramenti na kutoshirki katika shughuli za uongozi wa kanisa .
Alisema "ikiwa aliyetengwa atahudhuria au atakuwepo katika mazingira ya inapofanyika ibada, lazima aondoke au au kama hatatoka, ibada itasitishwa. Na ikiwa atakufa bila kutubu, hatapewa maziko ya kanisa," alisema Padri Katonto.
Padri Kantonto alisema kundi la pili ni la waumini waliowekewa pingamizi ambao hata hivyo, hakutaja idadi yao.

Alisema chini ya pingamizi walilowekewa, waumini hao wananyimwa haki ya kupata huduma za kanisa kwa muda, wakati makosa yao yakichunguzwa na kwamba kama itabainika kuwa hawakufanya, watarudishiwa huduma zote.

Alisema hata hivyo, pingamizi hilo haliwaondowi watu wa kundi katika umoja na kanisa, kama ilivyo kwa waliotengwa.

Alisema katika kipindi cha uchaguzi mkuu, kanisa lilijitahidi kuwakumbusha waumini wake kuhusu nafasi zao na wajibu wao, lakini kinyume chake kanisa limeshuhudia, na kusikia baadhi ya waumini wakionyesha utovu wa nidhamu kwa kukufuru utatu mtakatifu.

"Walikufuru utatu mtakatifu, baadhi ya wagombea wakajifafanisha na Mungu mwenye nafsi tatu, kukufuru msalaba mtakatifu wa kanisa kwa kuuzika, kukejeli, kutukana na kudharau viongozi wa kanisa na wakristo wenzao," alisisitiza Padri Katonto.

Alisema vitendo hivyo vimesikitisha mno mama kanisa kwa sababu vimeambatana na usaliti wa imani na maadili ya kikristo.

"Lakini pia vitendo hivyo ni makwazo kwa wana kanisa na wakristo wa madhehebu mengine na watu wote wenye mapenzi mema," alisema.
Alisema wanaotenda makosa kama hayo kwa mujibu wa sheria, kanisa, lina haki ya msingi ya kuwaadhibu na kwamba adhabu hizo si ngeni ndani ya kanisa.
Kasisi huyo alifafanua kuwa shutuma dhidi ya kanisa kuwa limewatenga na kuweka pingamizi waumini wake kwa sababu za itikadi za kisiasa ikiwa ni pamoja na kuipigia kura CCM ni uwongo na uzushi wenye lengo la uchochezi.

"Kanisa Katoliki linahoji hivi uchochezi huo unafanywa kwa maslahi na manufaa ya nani," alisema.
Alisisitiza kuwa kamwe kanisa halitokaa kimya bila kukemea uovu kwa hofu ya vitisho na uzushi unaolenga katika kutetea maslahi ya kundi la watu wachache wasio na dhamira safi

No comments:

Post a Comment